RAIS John Magufuli amempendekeza na kumteua tena Mbunge wa Ruangwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu Mstaafu, Kassim Majaliwa Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mpambe wa Rais Magufuli amewasilisha kwenye Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bahasha ya Rais Magufuli yenye jina pendekezwa la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Jina hilo limesomwa hii leo Novemba 12, 2020, Bungeni Dodoma na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai, mara baada ya jina hilo kuwasilishwa na mpambe wa Rais.
“Barua hii imetoka kwa Mh. Rais na kuelekezwa kwangu mimi Spika wa Bunge, na imeandikwa kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kushika madaraka yake ndani ya siku 14, atamteua mbunge wa kuteuliwa anayetokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi kuwa Waziri Mkuu, kwa kutekeleza matakwa ya katiba nimemteua Mheshimiwa mbunge wa Ruangwa, Kassim Majaliwa”, amesema Spika Ndugai, wakati akisoma barua ya Rais Magufuli.
Aidha Spika Ndugai ameongeza kuwa, “Mh Rais ameleta jina la Kassim Majaliwa, ili uteuzi wake uthibitishwe na Bunge tukufu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Kilichofuata ni wabunge kupitisha jina hilo la Waziri Mkuu Mteule kwa kulipiga kura ya NDIYO au HAPANA ambapo iwapo atapitishwa na Bunge hilo, basi atakuwa Waziri Mkuu kwa muhula wa pili wa awamu ya nne ya uongozi wa Magufuli. Majaliwa alianza kukitumikia cheo hicho 2015-2020 na sasa akipitishwa utakuwa muhula wa pili wa 2020-2025.
Post A Comment:
0 comments: